Wanawake wengi zaidi katika maeneo ya mijini wanabeba jukumu la kutoa maamuzi katika kaya zao. Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya na Idadi ya Watu nchini Kenya (KDHS) 2022, unaonesha kuwa idadi ya kaya zinazoongozwa na wanawake katika maeneo ya mijini imeongezeka kutoka asilimia 27 hadi 31 katika miaka minane iliyopita. Katika ngazi ya kitaifa, theluthi moja ya kaya nchini Kenya bado zinaongozwa na wanawake, kama ilivyokuwa mwaka 2014.
Sawa na ripoti ya mwaka 2014, kaya zinazoongozwa na wanawake zinapatikana zaidi katika maeneo ya vijijini kwa asilimia 36. Sababu zinazochangia kaya hizi kuongozwa na wanawake ni pamoja na kutengana, talaka au ujane. Ripoti inaonesha kuwa kwa ujumla, asilimia ya wanawake waliotengana au kuachwa ni karibu mara mbili ya wanaume kwa asilimia 11 ikilinganishwa na asilimia tano kwa wanaume. Hivyo leo katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia nafasi ya mwanamke katika familia hasa ya kuongoza na kutoa maamuzi.