Elimu ama Utajiri unahusiana na unene na wembamba?
2023-07-28 08:00:28| CRI

Unene ni moja ya sababu kuu za hatari kwa magonjwa mengi sugu, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo, ugonjwa sugu wa figo, ugonjwa wa kisukari na saratani mbalimbali. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kuboreshwa kwa lishe, na mabadiliko ya tabia ya maisha, kiwango cha uzito kupita kiasi na unene kinaongezeka kwa udhahiri, huku kiwango cha unene wa wanawake wa vijijini pia kikiongezeka.

Jarida la the Lancet la Uingereza ambalo ni jarida la kimataifa la afya, limechapisha utafiti uliofanywa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha China ambacho kilifanya uchambuzi wa kina juu ya afya ya watu zaidi ya laki 7.4 kati ya mwaka 2004 na 2018. Utafiti huo umegundua kuwa, tokea mwaka 2004 hadi 2018, wastani wa Kiwango cha Molekuli ya Mwili (BMI) cha China uliongezeka kutoka 22.7 hadi 24.4, na kiwango cha watu wanene wenye magonjwa kimeongezeka kutoka asilimia 3.1 hadi asilimia 8.1, huku idadi ya watu wanene wenye umri wa miaka 18 hadi 69 katika mwaka 2018 ilikuwa milioni 85, na kuongezeka mara tatu ikilinganishwa na mwaka 2004.

Utafiti huo pia umegundua kuwa, kiwango cha unene kinahusiana na kiwango cha elimu, ambapo watu wenye elimu ya juu zaidi wana kiwango cha chini zaidi cha BMI, hali hii imethibitishwa katika maisha halisi, na kinyume chake, wale wenye shahada ya chini wana uwezekano mkubwa zaidi kuwa na kiwango cha juu zaidi cha BMI. Chuo Kikuu cha Vanderbilt nchini Marekani kilifanya utafiti na kuonesha kuwa, hakuna uwezekano mkubwa kwa wanawake wenye uzito mkubwa kupita kiasi kupata ajira yenye mshahara wa juu. Hivyo leo katika Kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutajadili swali hili kwamba Je Elimu ama Utajiri unahusiana na unene na wembamba?