Umoja wa Mataifa umesema mapigano nchini Sudan yameendelea kusababisha ongezeko la kasi la wakimbizi wa ndani.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja huo Stephane Dujarric amenukuu takwimu mpya zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) zinazoonyesha kuwa, wiki iliyopita pekee, karibu watu 200,000 walikimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo. Amesema mashirika ya kibinadamu nchini Sudan yameendelea kutoa misaada kwa watu wanaokimbia mapigano hayo, na kuongeza kuwa, ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa wahitaji nchini humo bado unakabiliwa na changamoto nyingi.
IOM imesema, tangu kuanza kwa mapigano nchini Sudan miezi mitatu iliyopita, zaidi ya watu milioni 2.6 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini humo.
Wakati huohuo, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema, zaidi ya watu 730,000 wamekimbilia katika nchi jirani na Sudan.