Tanzania yawataka wananchi kuwapuuza wanaopinga uwekezaji wa bandari
2023-07-19 10:40:52| cri

Serikali ya Tanzania imewataka wananchi kuwapuuza watu wanaopinga uwekezaji unaofanywa na serikali katika bandari ya Dar es Salaam.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amesema hayo baada ya kuzindua shina la Ushirika la Umoja wa Vijana wa Ikwiriri wilayani Rufiji.

Amesema mpango wa uwekezaji unaofanywa na Serikali katika bandari hiyo unakwenda kuingiza mapato makubwa ambayo yatasaidia kusukuma sekta nyingine ukilinganisha na mapato kidogo yanayopatikana sasa.

Aidha, amewasihi watu wenye hoja za msingi kuziwasilisha serikalini ili zifanyiwe kazi badala ya kuwadanganya wananchi kwa tamaa zao za kutaka kushika dola.