Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Gilead Teri, amesema kituo hicho kinapanga kusajili idadi kubwa ya miradi mipya ya uwekezaji kwa mwaka huu. Akiongea na wanahabari Bw. Teri amesema tayari TIC imesajili miradi 229 yenye thamani ya dola bilioni 2.2 (takriban Sh5.15 trilioni) katika kipindi cha kwanza cha mwaka huu, miradi inayotarajiwa kutoa nafasi 31,647 za ajira.
Amesema mwaka jana TIC ilisajili jumla ya miradi mipya 293 yenye thamani ya dola bilioni 4.54 (Sh10.62 trilioni), na katika nusu ya pili ya mwaka huu, Kituo kina kazi ndogo ya kuvutia miradi 64 zaidi kufikia takwimu sawa zilizosajiliwa mwaka jana.
Amesema sheria mpya ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2022 imeweka mazingira wezeshi ya biashara yanayowafanya wawekezaji kuiona Tanzania kuwa ni sehemu bora ya uwekezaji.
Sheria mpya imepunguza kiwango cha chini cha mtaji wa uwekezaji kwa biashara inayomilikiwa na Mtanzania kutoka dola laki 1 hadi dola elfu 50, na kwa wageni kinabaki kuwa dola laki 5.