Kamati ya Umoja wa Afrika yatoa wito wa kurejeshwa kwa makubaliano yaliyositishwa ya usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi
2023-07-20 08:27:55| CRI

Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat amezitaka pande zinazohusika kurejesha makubaliano ya usafirishaji wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi.

Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter, Mahamat amesema anasikitishwa na kusitishwa kwa Pendekezo la Bahari Nyeusi, ambalo Umoja wa Afrika umekuwa ukilitetea, na kuzitaka pande husika kutatua masuala yoyote yaliyojitokeza na kurejesha usafiri salama wa nafaka na mbolea kutoka Ukraine na Russia kufikia maeneo yanayohitaji, hususan barani Afrika.

Mwezi Julai mwaka jana, Russia na Ukraine kwa nyakati tofauti zilisaini Pendekezo la Usafirishaji wa Nafaka kupitia Bahari Nyeusi pamoja Uturuki na Umoja wa Mataifa, ambalo liliiruhusu Ukraine kusafirisha nafaka zake na bidhaa nyingine za kilimo kupitia bandari zake zilizoko kwenye Bahari Nyeusi.

Hata hivyo, jumatatu wiki hii, Russia ilitangaza kuwa inasitisha ushiriki wake katika Pendekezo hilo, ikisema sehemu ya Pendekezo hilo inayohusiana na Russia haikutekelezwa.