Serikali ya Tanzania imesema inalenga kupunguza ukosefu wa ajira kutoka asilimia 9 (mwaka 2019) hadi asilimia 8 ifikapo 2025/26 kupitia Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Dk Joyce Ndalichako amesema kuhimiza upatikanaji wa ujuzi ni moja ya mikakati itakayotumiwa na serikali kufikia lengo hilo.
Amesema serikali pia itaongeza idadi ya wahitimu wanaopata mafunzo kazini ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza ujuzi kwa vijana.
Dk. Ndalichako amesema wanaamini kuwa suluhisho la ukosefu wa ajira litatokana na ushirikiano wa kutosha kati ya serikali na waajiri. Amesema kupitia Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26), Serikali inatarajia kuongeza idadi ya wahitimu wa mafunzo ya kazi kutoka 46,000 mwaka 2019/20 hadi laki 2.3 ifikapo 2025/26. Kwa upande wa mafunzo lengo ni kuongeza idadi ya wahitimu kutoka 30,000 ya mwaka 2019/20 kufikia wahitimu laki 1.5 ifikapo mwaka 2025/26.