Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekubali kushirikiana na Zimbabwe katika mradi mpya wa Mpango wa Kujisimamia (SMP), utakaoanza katika robo ya nne ya mwaka 2023.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana na Ofisi ya Usimamizi wa Madeni ya Umma iliyo chini ya Wizara ya Fedha na Maendeleo ya Uchumi ya nchini Zimbabwe.
Mpango wa Kujisimamia ni sehemu ya sera za kivitendo ambazo serikali ya Zimbabwe inatarajiwa kuzitekeleza chini ya mpango wa mchanganuo wa marupurupu na ulipaji wa madeni, ambao ulikubaliwa na wadeni wa pande nyingi na pande mbili mwezi Februari mwaka huu.
Katika lengo lake la kumaliza deni lake kubwa la nje, mwezi Desemba mwaka jana, serikali ya Zimbabwe ilianzisha Jukwaa la Utaratibu wa Majadiliano na wadeni wake wote, wenza wa maendeleo na wadau, na mpaka sasa, mikutano mitano imefanyika mjini Harare, kujadili masuala waliyokubaliana yanayojikita kwenye uchumi na mageuzi ya uongozi.