Serikali ya Kenya imesema itafanya kazi kwa karibu na wataalamu wa sekta ya nyuklia ili kuhakikisha viwango vya juu vya usalama wakati inaendelea na juhudi zake kuwa na kituo cha kwanza cha umeme wa nyuklia.
Haya yanajiri wakati Mamlaka ya Usimamizi wa Nyuklia ya Kenya (KNRA) imefikia makubaliano ya ushirikiano na kampuni moja ya nyuklia ya Marekani. Mwenyekiti wa KNRA Bw. Omondi Anyanga na Mkurugenzi Mkuu Bw. James Keter wamekutana na Bwana Donald Hoffman, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Excel Services, na kujadili mambo kuhusu udhibiti wa usalama.
Kampuni hiyo ya Marekani inasaidia wazalishaji wa umeme wa nyuklia kwenye mipango ya kuboresha usalama na usimamizi.
Bwana Hoffman amesema kutokana na mafunzo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 38 iliyopita, wameweza kujifunza mambo mazuri na changamoto zilizojitokeza katika nchi nyingine.