Tanzania kuzia uagizaji wa sukari nje ya nchi
2023-07-21 22:57:43| cri

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema mwishoni mwa mwaka ujao utakuwa mwisho wa Tanzania kuagiza sukari nje ya nchi kwa matumizi ya kawaida. Mpango huo wa Tanzania unalenga kuvilinda viwanda vya kuzalisha sukari nchini humo  pamoja na kupanua soko la viwanda vipya vya sukari vitakavyojengwa katika mikoa ya Mtwara, Mwanza, Dodoma na Kigoma. 

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa siku chache zilizopita na Mkurugenzi wa Benki ya Kilimo, Frank Nyabundege, Tanzania inazalisha tani 360,000 za sukari kwa mwaka wakati mahitaji ni tani 630,000.

Kutokana tofauti hiyo, kila mwaka Tanzania hulazimika kutoa vibali kwa ajili ya kuagiza sukari, hali ambayo imekuwa ikisababisha uhaba na kupanda bei kwa bidhaa hiyo.

Kando na kulinda soko la ndani, mpango huo pia unalenga  kuongeza nafasi za ajira hasa miongoni mwa vijana Watanzania na kuchochea shughuli za uzalishaji mali na uboreshaji wa miundombinu.