UM: Wafanyakazi 18 wa misaada wafariki katika siku 100 zilizopita tangu mgogoro wa Sudan uanze
2023-07-26 08:26:02| CRI

Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Farhan Haq amesema wafanyakazi wa misaada zaidi ya 18 waliuawa katika siku 100 zilizopita tangu mgogoro wa Sudan ulipoanza.

Kwa mujibu wa mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami, kati ya maelfu ya raia waliouawa au kujeruhiwa, ni wafanyakazi zaidi ya 18 wa kibinadamu waliouawa na wengine wengi waliojeruhiwa.

Msemaji huyo amesema wafanyakazi zaidi ya 24 wa kibinadamu walishikiliwa, na baadhi bado hawajulikani walipo. Maghala zaidi ya 50 ya misaada ya kibinadamu yaliporwa, ofisi zaidi ya 80 zilivamiwa, na magari zaidi ya 200 yaliibiwa.

Msemaji huyo pia amesema Shirika la Afya Duniani WHO limetahadharisha kuhusu kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya huduma za afya nchini Sudan, na zaidi ya asilimia 80 ya hospitali nchini humo zimesitisha huduma kutokana na mgogoro.