Mashindano ya nane ya ujuzi wa kiufundi barani Afrika yameanza jumatatu wiki hii katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia mjini Nairobi, Kenya. Mashindano hayo yameandaliwa na kampuni ya AVIC International ya China ikishirikisha Wizara ya Elimu ya Kenya na Shirikisho la Mawasiliano ya Kimataifa ya Elimu la China kwa, na kuvutia washiriki kutoka nchi tisa za Afrika ambazo ni Kenya, Cote d'Ivoire, Misri, Gabon, Ghana, Uganda, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mashindano hayo, Katibu mkuu wa vyuo vya mafunzo ya kiufundi nchini Kenya Dkt. Esther Muoria amesema, ushirikiano wa muda mrefu na kampuni ya AVIC International ya China umezifanya taasisi 154 za elimu za ufundi stadi nchini Kenya ziwe na vifaa vya kisasa, na kuiwezesha Kenya kuandaa wanafunzi wanaohitimu wenye uzoefu wa kazi, hivyo kusaidia nchi hiyo kuongeza idadi ya watu wanaopata nafasi za ajira na kuhimiza mchakato wa viwanda.
Amewataka washiriki wa mashindao hayo watumie vizuri fursa hiyo na kuongeza uwezo wao wa kazi, na kutoa mchango katika kutatua changamoto zinazoikabili Afrika na dunia.