Jumuiya ya maendeleo ya kiserikali ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD), imesema ushiriki wa wanawake kutoka jamii za watu wanaoishi kwa kuhamahama, utakuwa mchango muhimu katika kuleta mabadiliko ya sekta ya mifugo na kuchochea ukuaji shirikishi katika Pembe ya Afrika.
Ofisa wa IGAD anayeshughulikia Mifugo na Uvuvi, Bwana Ameha Sebsibe, amesema kutumia maarifa ya jadi na werevu walionao wanawake wafugaji, kutaongeza uhai katika sekta ya mifugo inayosaidia mamilioni ya watu katika ukanda huo.
Bwana Sebsibe amezitaka nchi za Pembe ya Afrika kupitisha sera za uzalishaji wa mifugo unaostahimili mabadiliko ya tabia nchi, na kuzingatia mahitaji ya usafi katika kuimarisha biashara ya kuvuka mpaka ya nyama, maziwa na ngozi.