Jumuiya ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini imeomba fedha za dharura za dola milioni 26.4 za kimarekani kuunga mkono usafirishaji wa watu wanaokimbia mapigano nchini Sudan kwenda Sudan Kusini hadi mwishoni mwa mwaka huu.
Kaimu Mratibu wa maswala ya kibinadamu nchini Sudan Kusini Bw. Peter Van der Auweraert amesema, wengi kati ya waliofika nchini Sudan Kusini wanakabiliwa na hali duni zaidi kutokana na kutokuwa na chanzo cha kifedha kuendelea na safari zao.
Bw. Auweraert ametoa taarifa huko Juba ikisema fedha zinapungua kwa kasi, na bila fedha mashirika ya kibinadamu yatalazimika kusimamisha msaada wa usafirishaji ndani ya wiki mbili.
Jumuiya hiyo pia imesema, tangu mgogoro wa Sudan ulipuke Aprili 15, watu zaidi ya 193,000 wamevuka mpaka na kuingia Sudan Kusini.
Habari nyingine kutoka Shirika la Uhamiaji la Kimataifa IOM zinasema, idadi ya watu wanaoingia Ethiopia kutoka Sudan inakaribia elfu 70.