Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa aongoza kikao cha 77 cha Bodi hiyo
2023-07-27 11:02:55| cri

Kikao cha 77 cha Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBoA) kimefanyika kuanzia Julai 25 hadi 26 kwenye Makao Makuu ya Umoja huo mjini New York, Marekani.

Kikao hicho kilichoongozwa na Hou Kai, ambaye ni mwenyekiti wa UNBoA na mkaguzi mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya China, kilijadili na kupitisha ripoti 21 za ukaguzi wa hesabu za mashirika na miradi ya Umoja wa Mataifa katika mwaka wa fedha wa 2022. Pia kilijadili masuala yaliyoletwa kwenye Bodi hiyo na chombo cha utungaji sheria cha Umoja wa Mataifa, na kupanga kazi za Bodi ya Ukaguzi katika nusu ya pili ya mwaka 2023.

Katika kikao hicho, wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi walifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Guterres na kubadilishana mawazo kuhusu masuala makubwa yaliyogunduliwa katika ukaguzi wa hesabu za Umoja wa Mataifa mwaka 2022, pamoja na vipaumbele muhimu na changamoto zinazoukabili Umoja wa Mataifa.

Hou Kai amesisitiza kwamba, Umoja wa Mataifa unabeba jukumu muhimu katika kuhimiza amani na maendeleo ya binadamu, na Umoja wa Mataifa wenye nguvu unahitajika katika kujenga jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.

Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa ni chombo huru cha wataalam ambacho kina jukumu muhimu katika mfumo wa usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kama utaratibu muhimu wa kukuza uwajibikaji na uwazi wa Umoja wa Mataifa.