Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetoa wito wa juhudi za pamoja katika kumaliza usafirishaji haramu wa watu kutoka Pembe ya Afrika kwenda nchini Yemen na nchi nyingine za Ghuba.
Shirika hilo limezitaka serikali, vyombo vya usalama, mashirika ya kijamii na huduma za jamii kuongeza juhudi katika kuzuia, kutambua na kuwasaidia wahanga na manusura, na kumaliza biashara haramu ya binadamu.
Katika taarifa iliyotolewa jana mjini Nairobi, Kenya, Shirika hilo limesema watu milioni 36.6 katika nchi za Ethiopia, Somalia, Kenya na Djibouti wameathirika na biashara hiyo, na kuongeza kuwa, wahamiaji wengi wanajikuta wakiangukia mikononi mwa wafanyabiashara hao.
Kwa mujibu wa Shirika hilo, wanawake na wasichana wameendelea kuwa kundi lililo hatarini Zaidi, likichukua asilimia 70 ya waathirika wa biashara ya binadamu.