Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amewataka viongozi wenzake wa Afrika kuunganisha nguvu katika kuwekeza kwenye maendeleo ya raslimali watu.
Akiongea mjini Dar es salaam kwenye ufunguzi wa mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu mtaji wa raslimali watu, Rais Samia amesema wakati umefika, na inawezekana kuwekeza katika raslimali watu kwa kuunganisha nguvu.
Kwenye mkutano huo ulioandaliwa na Tanzania kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, Rais Samia alikumbusha kuwa ongezeko la idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi barani Afrika, linaweza kuwa msaada kama vijana watawezeshwa kwa afya, elimu na ujuzi wanaohitaji ili kufikia uwezo wao kamili na kuchangia maendeleo ya kanda.
Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya wajumbe 2,000 kutoka nchi 44 za Afrika, wakiwemo wakuu wanane wa nchi na serikali, makamu wa rais, mawaziri wakuu na mawaziri.