Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ahimiza kuachiliwa kwa rais wa Niger
2023-07-28 08:58:59| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres ametaka kuachiwa mara moja na bila masharti kwa Rais wa Niger Mohamed Bazoum, wakati Umoja huo umesimamisha shughuli za kibinadamu nchini Niger kutokana na hali ilivyo sasa.

Taarifa iliyotolewa jumatano jioni na wizara ya ulinzi ya Niger, ilisema wanajeshi wa nchi hiyo wamemwondoa madarakani Bw. Bazoum, saa chache baada ya kumuweka rais huyo kizuizini.

Akihutubia mkutano na wanahabari mjini New York, Bw. Guterres ametaka wanaomzuia Rais Bazoum kumwachia huru mara moja na bila masharti, kuacha kukwamisha utawala wa kidemokrasia na kuheshimu utawala wa sheria.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric pia amesema kwenye mkutano na wanahabari kuwa kutokana na hali ilivyo sasa nchini Niger, Umoja wa Mataifa umesitisha operesheni zake za kibinadamu.