Kenya yazindua maabara ya kwanza ya utafiti wa seli shina ili kukabiliana na magonjwa
2023-07-28 08:59:40| CRI

Kituo kikuu cha utafiti nchini Kenya kimezindua maabara ya kwanza ya utafiti wa seli shina (stem cell) ili kusaidia kuendeleza matibabu na kuzuia Magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs).

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya (KEMRI) Bw. Elijah Songok, amesema maabara hiyo ambayo ni maabara ya kwanza kabisa katika eneo la Afrika kusini mwa Sahara, itasaidia maendeleo ya teknolojia mpya za matibabu na kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Bw. Songok amebainisha kuwa utafiti wa seli shina utatuwezesha kutengeneza matibabu ya kurejesha na kurekebisha tishu ambazo zimeharibiwa au kuathiriwa na magonjwa au ajali kama vile saratani, kisukari, kuungua, majeraha ya uti wa mgongo.