Waziri Mkuu wa China akutana na rais wa Mauritania
2023-07-31 10:10:32| CRI

Waziri Mkuu wa China Li Qiang amekutana na Rais wa Mauritania Mohamed Ould Cheikh Ghazouani jana Jumapili hapa Beijing.

Katika mazungumzo yao Li amesema China na Mauritania, zote mbili zikiwa ni nchi zinazoendelea, zimekuwa na misimamo sawa katika masuala mengi ya kimataifa na kikanda, zinaungana mkono na kujenga urafiki wa dhati. Wakuu wa nchi hizo mbili walikuwa na mkutano uliozaa matunda na kwa pamoja wakaweka mipango mipya ya kuendeleza mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Aidha Bw. Li amesema China inapenda kushirikiana na Mauritania kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kuendeleza urafiki wa jadi, kutafuta ushirikiano zaidi katika mikakati ya maendeleo, kubadilishana uzoefu wa maendeleo na mafanikio, na kusukuma mbele uhusiano wa kirafiki wa ushirikiano kati ya China na Mauritania ufikie kwenye ngazi mpya.

Rais Ghazouani alibainisha kuwa uhusiano kati ya Mauritania na China unatokana na kuheshimiana, kunufaishana na kupata matokeo mazuri, akisema urafiki wa nchi hizo mbili ni wa kina na thabiti. Pia Mauritania inaishukuru China kwa kuiunga mkono kwenye uhuru na maendeleo yake, na inakubaliana kikamilifu na Mpango wa Maendeleo ya Dunia, Mpango wa Usalama wa Dunia na Mpango wa Ustaarabu wa Dunia.