ECOWAS yawawekea vikwazo viongozi wa kijeshi wa Niger baada ya mapinduzi
2023-07-31 10:13:40| CRI

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), inayojumuisha nchi 15 wanachama, imekubaliana kuwawekea vikwazo viongozi wa kijeshi wa Niger waliohusika katika mapinduzi ya hivi karibuni katika mkutano wa dharura uliofanyika Jumapili huko Abuja.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye pia ni mwenyekiti wa Mamlaka ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa ECOWAS, alikemea mapinduzi hayo, akisema jumuiya hiyo "inakataa mapinduzi na kukatizwa kwa utaratibu wa kikatiba."

Tinubu  alisema kuwa  wakiwa viongozi wa Afrika, ni jukumu lao kuimarisha utulivu na maendeleo, akibainisha kuwa ECOWAS inatetea juhudi za pamoja za kuzuia mapinduzi katika bara la Afrika.

Kwenye taarifa yake jumuiya hiyo ilisema jeshi la Niger lazima litoe mamlaka ndani ya wiki moja, kumwachilia mara moja na kumrejesha madarakani rais Mohamed Bazoum aliyechaguliwa wa nchi hiyo, la sivyo ECOWAS itachukua hatua zote zinazohitajika kurejesha utulivu wa kikatiba nchini Niger, pamoja na matumizi ya nguvu. Aidha viongozi hao walikubaliana kuweka vikwazo vya kifedha na usafiri kwa viongozi wa kijeshi wa Niger walioshiriki katika mapinduzi hayo, na pia kutoruhusu kupiga marufuku usafiri wa ndege za kibiashara kwenye eneo la nchi  hiyo. Pia waliamua kufunga  mali za Niger katika benki kuu na za kibiashara za nchi za ECOWAS.