Xi asema China itashirikiana na Pakistan kujenga mradi wa CPEC kuwa mfano wa ushirikiano wa hali ya juu wa Ukanda Mmoja Njia Moja
2023-08-01 09:34:54| CRI

Rais Xi Jinping wa China amesema China itashirikiana na Pakistan ili kulenga matokeo ya hali ya juu, endelevu na ya kuboresha maisha, pamoja na kujenga zaidi Ukanda wa Kiuchumi wa China na Pakistani (CPEC) kuwa mradi wa kupigiwa mfano wa ushirikiano wa hali ya juu wa Ukanda Mmoja Njia Moja.

Xi ameyasema hayo katika salamu za pongezi alizozitoa Jumatatu kwenye hafla ya maadhimisho ya kutimia Muongo mmoja wa Ukanda wa Kiuchumi wa China na Pakistani iliyofanyika mjini Islamabad, Pakistan. Xi alisema CPEC ni mradi muhimu wa mwanzo wa ushirikiano wa Ukanda Mmoja Njia Moja. Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2013, China na Pakistan zimekuwa zikiendeleza CPEC chini ya kanuni ya mashauriano ya kina, kuchangia na kunufaika kwa pamoja, na zimepata matokeo kadhaa ya mapema.

Akisisitiza kuwa China na Pakistan zitaendelea kuboresha mipango ya jumla na kupanua na kuimarisha ushirikiano, Xi alisema bila kujali mazingira ya kimataifa yatabadilika namna gani, China daima itasimama kidete na Pakistan.