ATMIS yasema awamu ya kwanza ya kupunguza askari wake nchini Somalia imefanyika kwa mafanikio
2023-08-01 23:06:24| cri

Makamanda wa Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) wamekamilisha mkutano wa siku nne kutathmini awamu ya kwanza ya kuondoa askari wake nchini Somalia, ambayo wanasema imetekelezwa kwa mafanikio mwezi Juni.

Tume hiyo imesema, mkutano huo uliofanyika mjini Mogadishu jana jumatatu, ulihudhuriwa na makamanda wa vikosi vya nchi tano zilizotoa askari wake, ambazo ni Kenya, Uganda, Djibouti, Ethiopia na Burundi.

Kamanda wa ATMIS, Sam Okiding, ambaye aliongoza mkutano huo, amesema walijadili masuala kadhaa ikiwemo hali ya usalama na matishio yanayotokana na kundi la al-Shabaab, na kufikia maazimio yatakayotekelezwa na makamanda wa maeneo husika.

Hivi sasa, ATMIS inapanga awamu ya pili ya operesheni ya pamoja ya kijeshi dhidi ya kundi la al-Shabaab, kufuatia kukamilika kwa awamu ya kwanza ya operesheni hiyo, ambayo ilikomboa maeneo mengi ya katikati na kusini mwa Somalia ambayo yalikuwa yakikaliwa na kundi hilo.