Masuala ya Afrika kujadiliwa katika mkutano ujao wa BRICS
2023-08-01 09:36:14| CRI

Idara ya Biashara, Viwanda na Ushindani ya Afrika Kusini ilisema Jumatatu kwamba nchi hiyo itatetea mafungamano ya bara la Afrika na kujadili masuala ya Afrika katika mkutano ujao wa BRICS unaojumuisha nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.

Kwenye taarifa yake idara hiyo imesema Afrika Kusini inakwenda kwenye mkutano huo ikiwa na lengo la kuweka ajenda ya Afrika mbele na kuwa na mazungumzo mazito kuhusu masuala ya Afrika. Ikiwa nchi mwenyekiti wa mkutano wa 2023 wa BRICS, Afrika Kusini imewaalika wakuu wa nchi zote za Afrika kwenye mkutano huo utakaofanyika Agosti 22 na 24 mjini Johannesburg.

Kwa mujibu wa taarifa, mkutano huo utajadili masuala ya Afrika ya kuwa na mauzo mseto ya nje kuelekea biashara ya ongezeko la thamani, kuongeza uwezo wa uzalishaji, kuongeza fursa za ujasiriamali na kugawana ujuzi, kuharakisha ukuaji na kuongeza thamani katika bara la Afrika.

Aidha idara hiyo imebainisha kuwa masuala ya kuongeza mtiririko wa uwekezaji barani Afrika, kuongeza uhamishaji wa teknolojia, fursa za ajira, na kuboresha mapato pia yatajadiliwa katika mkutano huo.