Serikali ya Kenya itaanza kukarabati maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kote nchini humo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu wa mavuno utakaoanza Oktoba mwaka huu.
Katika taarifa yake iliyotolewa Jumapili jioni, Mkuu wa Utumishi wa Umma katika Ikulu ya Kenya, Felix Koskei, amesema serikali pia itakarabati mitambo 36 ya kukausha nafaka kando na kununua mingine 70, na kuongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali za kupunguza hasara ambayo wakulima hupata baada ya mavuno.
Aidha, Bw Koskei amesema serikali kuu na serikali za kaunti zitakarabati barabara katika eneo la North Rift, zikiwemo zile za vijijini ili kuwawezesha wakulima kusafirisha mahindi yao katika maghala ya NCPB kwa urahisi.