Walinda amani wa Uganda waanza kuondoa mabomu ambayo hayajalipuka nchini DR Congo
2023-08-02 08:51:53| CRI

Wanajeshi wa kulinda amani wa Uganda wameanza kazi ya kutegua na kuondoa mabomu ambayo hayakulipuka huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu huko Kampala, UPDF ilisema Kitengo cha Uteketezaji wa Mabomu (EOD) cha Kikosi cha Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Uganda (UPDF) kinaondoa silaha ambazo hazijalipuka kwenye maeneo kadhaa ya mashambani na vichakani ndani ya vijiji vya Mabenga katika Mkoa wa Kivu Kaskazini.

Hadi sasa kikosi hicho kimeondoa kwa usalama vipande mbalimbali 18 vya mabomu ambayo hayajalipuka, kuanzia mabomu ya kurushwa kwa roketi (RPG), mabomu ya vifaru vikuu vya vitani, mabomu ya kuzuia vifaru, mabomu ya milimita 82, fyuzi za mabomu, mabomu ya kurushwa kwa mkono na risasi za aina mbalimbali za bunduki za kivita.

Afisa mkuu wa kikosi cha 9, Samuel Mawanda Lubega, alisema Kikosi cha UPDF kina wajibu wa kuwalinda raia dhidi ya hatari za mabomu ambayo hayajalipuka, akibainisha kuwa baadhi ya mabomu yalikuwa bado yanafanya kazi na yangesababisha hatari kubwa kwa maisha ya binadamu na wanyama kama yakichezewa.