Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu imetoa taarifa ikisema kwamba hatua ya Kenya ya kurejesha shughuli za ukataji miti katika misitu ya umma inalenga kuleta uwiano kati ya juhudi za uhifadhi na ukuaji wa uchumi
Wizara hiyo imefafanua kuwa inalenga kuvuna miti kwenye eneo la hekta 26,000 za misitu ya umma ili kutoa fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini. Taarifa hiyo imesema miti hiyo isipoondolewa mwisho itaoza na kufa hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mapato ambayo yangetumika katika kurejesha misitu iliyoharibika.
Rais wa Kenya William Ruto mwezi Mei aliondoa katazo la ukataji miti lililodumu kwa miaka sita, jambo ambalo liliibua hasira kwa wananchi. Wanamazingira walisema kuondolewa kwa katazo hilo kutarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika uhifadhi wa misitu wakati nchi inapokabiliwa na athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na ukame.