Rais wa China atuma salamu za rambirambi kwa mwenzake wa Pakistan kufuatia shambulizi la bomu la kujitoa muhanga
2023-08-02 08:48:33| CRI

Rais Xi Jinping wa China ametuma salamu za rambirambi kwa mwenzake wa Pakistan rais Arif Alvi kutokana na shambulizi baya la bomu la kujitoa muhanga lililowakumba watu waliokusanyika katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa nchini Pakistan.

Akiwa kwa niaba ya serikali ya China na watu wake, rais Xi aliomboleza kwa huzuni kubwa vifo vya watu waliouawa na kutuma salamu za dhati za rambirambi kwa familia zilizofiwa na wale waliojeruhiwa.

Xi amesisitiza kuwa China inapinga aina zote za ugaidi, na inalaani vikali shambulizi hilo. Pia ameahidi kuwa China itaendelea kuunga mkono kithabiti juhudi za Pakistan za kuhimiza mpango wake wa kitaifa wa kupambana na ugaidi na kulinda kwa pamoja amani na usalama katika kanda na dunia.

Kundi la IS Jumatatu lilitangaza kuhusika na shambulizi hilo la kujitoa muhanga lililotokea Jumapili katika mkusanyiko huo wa kisiasa, ambalo limesababisha vifo vya watu 54 na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa.