Nchi za Afrika zahimizwa kujenga miundombinu imara na salama ya kidijitali ili kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni
2023-08-02 08:53:07| CRI

Wajumbe waliohudhuria mkutano wa teknolojia ya mtandaoni Afrika ‘Cybertech’ uliofanyika siku ya Jumanne huko Kigali, Rwanda, walitoa wito kwa nchi za Afrika kujenga miundombinu imara na salama ya kidijitali ili kukabiliana na mashambulizi ya usalama mtandaoni na uhalifu unaohusika nao.

Wito huo wameutoa katika ufunguzi wa mkutano huo ambao umevutia zaidi ya wajumbe 1,500 kutoka kote barani Afrika na kwingineko, wakiwemo maofisa wa serikali, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, na wataalamu wa mifumo ya ikolojia ya mtandao.

Waziri wa TEHAMA na Ubunifu wa Rwanda, Paula Ingabire, alisema  kwenye ufunguzi huo wa mkutano kwamba wakati dunia inazidi kwenda mtandaoni, ndivyo wahalifu wa mtandao wanavyoongezeka. Akisema kuna haja kwa nchi za Afrika kushughulikia ipasavyo ili kulinda mustakabali wa pamoja wa kidijitali.

Alibainisha kuwa kujumuika pamoja na kubadilishana uzoefu ni muhimu kwa Afrika kuweza kukuza mbinu shirikishi ya kusimamia mtandao.