Watu wawili wauawa katika shambulio la Al-Shabaab nchini Kenya
2023-08-02 14:40:42| cri

Watu wawili wameuawa na wengine 10 wamejeruhiwa, akiwemo diwani wa Wadi ya Hindi, James Njaaga baada ya wapiganaji 60 wanaoshukiwa kuwa wa kundi la Al-Shabaab kufanya shambulio dhidi ya msafara wa magari katika eneo la Mwembeni, karibu na Lango la Simba kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, nchini Kenya.

Akithibitisha kutokea kwa shambulio hilo, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Profesa Kithure Kindiki amesema, shambulio hilo limetokea jana asubuhi, ambapo mtu mmoja aliuawa papo hapo na mwingine alifariki wakati akipelekwa hospitalini. Amesema maafisa wa usalama kutoka Nyangoro wamefika katika eneo la tukio upesi na wakawakabili magaidi waliokimbilia katika msitu wa Boni.

Shambulio hilo limetokea wiki tatu baada ya mtu mmoja kuuawa na nyumba tano kuchomwa moto na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab kwenye vijiji vya Salama na Widho, Lamu Magharibi.