Watu 20 wafa maji baada ya boti kuzama katika Ziwa Victoria nchini Uganda
2023-08-03 09:11:05| CRI

Takriban watu 20 wamekufa maji baada ya boti kupinduka katika Ziwa Victoria katikati mwa Uganda.

Kwenye taarifa fupi aliyoitoa kwa Xinhua, msemaji wa Polisi wa mji wa Kampala Patrick Onyango, alisema idadi ya watu waliokuwa kwenye boti inadaiwa kuwa 34, na tukio hilo lilitokea saa 11:00 asubuhi ambapo hadi sasa watu 20 wamethibitishwa kufariki.

Aliongeza kuwa boti hiyo iliyokuwa imebeba mkaa, vyakula vibichi na samaki ilikuwa ikisafiri kutoka visiwa vya wilaya ya kati ya Kalangala na kuelekea wilaya ya bara ya Wakiso Jumatano asubuhi. Chanzo cha ajali hiyo kimechangiwa na kujaza kupita kiasi na hali mbaya ya hewa.

Wakati huohuo waokoaji wamepata miili 12 ya watu waliozama baada ya boti mbili kupinduka katika Ziwa Victoria nchini Tanzania Jumapili jioni. Akifafanua kuhusu ajali hiyo, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania mkoani Mara Augustine Magere, alisema boti hizo zilikuwa zikisafirisha watu wapatao 28 waliokuwa wakirejea kijijini Bulomba baada ya maombi katika kanisa moja lililopo kijiji cha Mchigondo na kupinduka baada ya kukumbwa na dhoruba na kusababisha kifo cha mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na watu 13 kuzama. Magere alisema wengi wa wahanga hao ni watoto wa shule ya msingi Bulomba.