Tume ya UM yaeleza wasiwasi juu ya athari za mapigano kwa raia huko Darfur nchini Sudan
2023-08-04 09:54:38| CRI

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan (UNITAMS) Alhamisi ilitoa taarifa ikisema ina wasiwasi sana na athari mbaya kwa raia kutokana na mapigano kati ya vikosi vya msaada wa haraka (RSF) na vikosi vya jeshi la Sudan (SAF) katika mkoa wa Darfur.

Kwenye taarifa yake imelaani vikali shambulizi dhidi ya raia na vifaa vya umma lililofanywa na RSF ikishirikiana na wanamgambo wake kuanzia tarehe 24 hadi 26 Julai, hasa katika eneo la Sirba, kilomita 45 kaskazini mwa El Geneina jimboni Darfur Magharibi. Tume hiyo pia ilieleza wasiwasi wake juu ya matukio kama hayo yaliyotokea huko Nyala jimboni Darfur Kusini na Zalingei jimboni Darfur Katikati.

Kiongozi wa UNITAMS Bw. Volker Perthes alizikumbusha pande zote husika kutekeleza majukumu chini ya sheria ya kibinadamu ya kimataifa na sheria ya haki za binadamu ya kimataifa, ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa raia wote.