Serikali ya Tanzania imetenga jumla ya Sh bilioni 55.9 kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kuboresha huduma za tiba na shughuli za uendeshaji.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI, Prof. Abel Makubi wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi hiyo ndani ya miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita na Mipango ya mwaka 2023-2024. Amesema lengo ni kuongeza ubora wa huduma zote za ndani, ili kukidhi matarajio ya wananchi na kufikia viwango vya kimataifa, na kuongeza kuwa, Taasisi hiyo imeanzisha huduma mpya tatu za kibingwa bobezi, ambazo zinapunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu.
Ametaja matibabu hayo ya kibingwa kuwa ni tiba ya baadhi ya kiharusi, tiba ya baadhi ya vifafa, na upasuaji wa kiuno kwa njia ya matundu.
Ameeleza mipango mingine ni ukarabati wa miundombinu ya hospitali, ujenzi mpya miundombinu, ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD), ambalo litakuwa na vyumba 30 vya kliniki vya kisasa tofauti na vyumba saba vilivyopo sasa.