Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amesema huduma jumuishi za fedha ni miongoni mwa vipaumbele vya nchi, pia ni lengo muhimu la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Dkt. Mpango ameyasema hayo wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, katika hafla iliofanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam. Amesema kuwa huduma jumuishi za fedha ni nguzo muhimu inayopaswa kuzingatiwa kwa kuhakikisha watu wa makundi yote wanafikiwa.
Pia amesema, wataalam na wadau wa huduma jumuishi za fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wanatakiwa kuhakikisha wanaongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha hususani kwa vijana.