Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama--Kuwezesha Kunyonyesha: Kuleta Mabadiliko kwa Wazazi Wanaofanya Kazi
2023-08-04 08:49:35| CRI

Kuanzia Agosti Mosi hadi 7, dunia huadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama. Shirika la Afya Duniani na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa kwa pamoja yametoa takwimu zinazoonesha kuwa, chini ya nusu ya watoto wote wanaozaliwa, hunyonyeshwa katika saa ya kwanza ya maisha yao, na hivyo kuwaweka hatarini zaidi kukumbwa na magonjwa yanayoweza kuzuilika ama kufariki. Wakati huohuo, Baraza la Afya la Dunia liliweka malengo ya kunyonyesha watoto bila kuwapa kitu kingine chochote kwa miezi sita wafikie asilimia 50 ifikapo mwaka 2025. Lakini takwimu zilizotolewa zinaonesha ni asilimia 44 pekee ya watoto wachanga wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza ya maisha.

Idadi ndogo ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika kipindi hicho cha miezi sita inatokana na sababu kadhaa, ikiwemo waajiri kutowapa ruhusa waajiriwa wao wanawake kwenda kunyonyesha watoto wao, ama waajiri hao kutoa muda mfupi wa likizo ya uzazi, ambao ni chini ya miezi mitatu, ama pia huenda kutokana na ugumu wa maisha, wanawake wanaoruhusiwa kufanya kazi nusu siku na kwenda kunyonyesha watoto wao, wanaishia kwenda kufanya shughuli nyingine za kujiingiza kipato, na hivyo kuwakosesha watoto wao lishe bora wanayotakiwa kupata. Katika kipindi chetu cha leo cha Ukumbi wa Wanawake, tunaangazia zaidi haki za mwanamke mwajiriwa katika kunyonyesha pindi anapojifungua.