Trump akana mashtaka kwa kujaribu kupindua matokeo ya uchaguzi wa 2020
2023-08-04 09:59:53| CRI

Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amekana mashtaka ya kupanga njama ya kupindua uchaguzi wa rais wa 2020.

Trump alifikishwa mahakamani mjini Washington, D.C, Alhamisi mchana, siku mbili baada ya kufunguliwa mashtaka rasmi. Akiwa mbele ya jaji Trump alikana makosa yake yote manne aliyoshtakiwa.

Baraza kuu la mahakama siku ya Jumanne lilimshtaki Trump kwa makosa manne ya jinai yakiwa ni pamoja na njama ya kuilaghai Marekani, njama ya kuzuia mchakato rasmi, na njama ya kutaka kuwanyima wapiga kura wa Marekani haki yao ya uchaguzi wa haki.

Trump ni rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu. Mbali na mashtaka ya kujaribu kupindua uchaguzi wa 2020, pia anakabiliwa na mashtaka katika kesi nyingine mbili.