Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Tanzania (TARI), imedhamiria kuondoa changamoto kwenye uzalishaji wa ngano, ili kuondoa mzigo mkubwa unaobebwa na serikali ya Tanzania wa kutumia fedha nyingi za kigeni kuiagiza kutoka nje ya nchi.
Mratibu wa zao la ngano katika taasisi hiyo kutoka kituo cha Selian Arusha, Bw. Ismail Ngolida amesema kwenye maonesho ya wakulima ya Nane Nane yanayoendelea mkoani Mbeya, kuwa mahitaji ya ngano kwa sasa ni tani milioni 1 kwa mwaka, lakini uzalishaji uliopo ni tani laki 1 tu, kwa hiyo kuna upungufu wa tani laki 9.
Ametaja baadhi ya mikakati ya serikali kuwa ni kuzalisha mbegu za kutosha pamoja na kuongeza maeneo ya uzalishaji wa ngano, ili ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe imejitosheleza kwa uzalishaji wa zao hilo.