Watu 30 wafariki katika ajali ya treni nchini Pakistan
2023-08-07 08:47:14| CRI

Watu 30 wamefariki na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika ajali ya treni iliyotokea jana mkoani Sindh, kusini mwa Pakistan baada ya mabehewa 10 ya treni ya abiria kuanguka.

Mkuu wa mkoa wa Sindh Syed Murad Ali Shah amethibitishwa idadi hiyo ya vifo, na kusema mabehewa tisa yameondolewa katika eneo la ajali, na kuongeza kuwa operesheni ya uokoaji inaendelea katika behewa moja lililobaki.

Waziri mkuu wa Pakistan Shahbaz Shariff ameeleza kuhuzunishwa na ajali hiyo, na kuzielekeza mamlaka husika kutoa huduma bora ya matibabu kwa watu waliojeruhiwa.

Treni ya mwendo kasi ya Hazara, yenye mabehewa kati ya 16 na 17 na kubeba abiria zaidi ya 1000, iliyokuwa ikitokea Karachi kwenda mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, ilitoka kwenye njia yake wakati ikivuka daraja la juu ya mto.