China yapinga Ufilipino kusafirisha vifaa vya kukarabati manowari yake mbovu kwenye bahari ya China
2023-08-08 23:32:30| CRI

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imepinga kitendo cha Ufilipino kusafirisha vifaa vitakavyotumiwa katika matengenezo makubwa ya manowari yake mbovu iliyoko kwenye bahari karibu na Miamba ya Ren’ai ambayo ni sehemu ya visiwa vya Nansha nchini China.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa, hukumu iliyotolewa kuhusu kesi ya Bahari ya Kusini ya China inakiuka sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya Bahari, na China haikubali wala kutambua hukumu hiyo.

Pia Wizara hiyo imesema, China imewasiliana na Ufilipino juu ya suala la Miamba ya Ren’ai kwa njia ya kidiplomasia, na kuitaka Ufilipino isisafirishe vifaa vitakavyotumiwa katika matengenezo makubwa ya manowari yake mbovu katika bahari ya China. Kinyume chake, Ufilipino ilishikilia kuendelea na hatua hiyo, na kusababisha hali kuwa mbaya zaidi. Walinzi wa Pwani ya China wamechukua hatua za kulinda mamlaka ya China na ya bahari kwa kufuata sheria.

Pia imesisitiza kuwa China iko tayari kuendelea kushughulikia vizuri masuala ya bahari na Ufilipino kupitia mazungumzo, ili kulinda kwa pamoja uhusiano kati ya pande hizo mbili na utulivu wa baharini.