Kampuni ya Huawei ya China imeanzisha mradi wa mwaka 2023 wa “Mbegu za Baadaye” nchini Zambia, kwa lengo la kuwaandaa watu wenye ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Maofisa kutoka serikali ya Zambia, Ubalozi wa China nchini Zambia, maofisa wa kampuni ya Huawei na wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini humo wanaoshiriki kwenye mradi wa mwaka huu wameshiriki kwenye hafla ya kuanzishwa kwa mradi huo. Idadi ya wanafunzi wanaoshiriki kwenye mradio huo imefikia 50, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa mradio huo nchini Zambia mwaka 2015.
Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa nchini Zambia, Felix Mutati, ameipongeza Huawei kwa mradi huo, akisema unaendana na mkakati wa serikali wa kuboresha ujuzi wa kidijitali, kuboresha ujasiriamali wa kidijitali, na kuwezesha mtiririko wa taarifa za kidijitali.
Kwa upande wake, balozi mdogo wa China nchini Zambia Meng Hao amesema, China inajivunia maendeleo ya TEHAMA na ujuzi wa TEHAMA kwa kuwa maendeleo ya teknolojia ni kichocheo cha maendeleo ya jamii na uchumi.