Waziri Mkuu wa Tanzania Bw. Kassim Majaliwa amezitaka benki kubuni huduma zaidi zenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wakulima wa Tanzania. Bw. Majaliwa ametoa wito huo wakati akitembelea banda la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) katika Maonesho ya Kilimo Nanenane yaliyofanyika mkoani Mbeya.
Bw. Majaliwa amesema utoaji wa mikopo yenye riba nafuu ya vifaa vya kilimo utasaidia kuchochea maendeleo ya kilimo kwa kuongeza kasi ya uzalishaji na kipato kwa wakulima, na kutolea mfano huduma kuhusu wakulima inayoruhusu benki kusaidia wakulima kupata mikopo ya vifaa muhimu vya kilimo.
Mkuu wa idara ya wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) wa NBC, Bw. Raymond Urassa, amesema kupitia ushirikiano na kampuni ya pembejeo za kilimo ya Agricom, tayari benki hiyo imetoa mikopo ya vifaa vya kilimo vyenye thamani ya Sh bilioni 2.3 kwa wakulima mbalimbali wa Tanzania.