Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) Bwana John Maige, amesema bodi hiyo imenunua tani 35,000 za mazao ya kilimo yakiwemo mahindi, mpunga, alizeti na maharage.
Akizungumza mkoani Mbeya kwenye maonesho ya Nanenane, Bwana Maige amesema mwaka huu walijiwekea malengo ya kutumia Sh bilioni 100 lakini mpaka sasa wametumia Sh bilioni 29, na wanaendelea na ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima katika vituo vyao mbalimbali vilivyopo Iringa, Arusha, Dodoma, Songea, Sumbawanga na Tunduma.
Amesema bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko inatoa fursa mbalimbali kwa wakulima zikiwemo za kuuza mazao, uwakala wa kuuza mazao na bidhaa.