Wataalamu wa Afrika wakutana nchini Kenya kujadili matumizi ya setilaiti kwa ajili ya usalama wa chakula
2023-08-09 08:39:47| CRI

Wataalamu wa Afrika wameanza mkutano wa siku tatu mjini Nairobi, Kenya, kujadili matumizi ya mawasiliano ya setilaiti ili kusaidia kuongeza usalama wa chakula katika bara hilo.

Mkutano wa 7 wa kimataifa wa Kituo cha Kikanda cha Ramani ya Rasilimali kwa Maendeleo (RCMRD) umewakutanisha zaidi ya washiriki 1,000, wakiwemo maofisa wa ngazi ya juu wa serikali na wanasayansi kutoka nchi 20 za Afrika, pamoja na maofisa kutoka Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, ili kutathmini njia za kutumia majukwaa ya ufuatiliaji wa dunia kuimarisha sekta za kilimo katika bara hilo.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, ofisa mwandamizi wa sayansi katika Tume ya Umoja wa Afrika, Mahaman Bachir Saley, amesema picha zinazopigwa na setilaiti zitasaidia serikali za nchi za Afrika kufuatilia mazao mashambani, na hivyo kuzisaidia katika mipango yao kutokana na uwezo wa kutabiri mavuno kwa wakulima.