Mapigano makali yametokea jumatatu kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha RSF katika mji wa Omdurman ulioko kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.
Jeshi la Sudan lilishambulia vituo vya kikosi cha RSF katika miji ya pembezoni ikiwemo Bait Al-Mal, Al-Shuhada na Al-Mulazemin, ambapo kikosi cha RSF kilijibu kwa mashambulio ya makombora, na kusababisha vifo vya raia na uharibifu wa nyumba zao.
Wahudumu wa afya katika maeneo hayo wamesema mashambulio ya kundi la RSF yamesababisha vifo vya watu watano katika eneo la al-Sharafiya.
Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Sudan zimeonyesha kuwa, tangu mapigano makali kati ya Jeshi la nchi hiyo na Kikosi cha RSF kutokea katika mji wa Khartoum na miji mingine tangu April 15 mwaka huu, na watu 3,000 wameuawa na wengine zaidi ya 6,000 kujeruhiwa.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, zaidi ya watu milioni tatu wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan tangu kuanza kwa mapigano hayo.