Ofisa wa Umoja wa Mataifa asema mgogoro wa Sudan hauna suluhisho lingine mbali na mazungumzo
2023-08-10 15:11:59| cri

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya Afrika Bi. Martha Bobby, amesema pande hasimu za mgogoro wa Sudan zinahitaji kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo na kukomesha vita haraka iwezekanavyo, na hakuna suluhisho lingine mbali na mazungumzo. Amesema kwa sasa mgogoro huo umedumu kwa zaidi ya siku 100, na hakuna upande uliopata ushindi wa uhakika. Hali katika maeneo mbalimbali ya Sudan bado ni tete, na mgogoro huo unaweza kuenea zaidi katika nchi nzima.

Bi. Bobby amekaribisha juhudi za Umoja wa Afrika, Shirika la Maendeleo la kiserikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) na Saudi Arabia kumaliza mgogoro huo, na kusema uratibu kati ya mifumo iliyopo ya upatanishi wa kimataifa na kikanda ni muhimu, na Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi kwa karibu na washirika wa kimataifa kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Mgogoro wa Sudan ulizuka karibu na Khartoum, tarehe 15 Aprili, na hatimaye kuenea katika maeneo mengine ya Sudan.