Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Benki Kuu ya Tanzania inaonesha kuwa ingawa uchumi wa dunia unakabiliwa na hali mbaya ya kifedha, hatari zinazohusiana na mabadiliko ya tabia nchi, mgogoro wa Ukraine, na athari za janga la Covid-19, athari ya hatari hizo kwa uchumi wa Tanzania zimeendelea kuwa ni za wastani.
Ripoti hiyo kuhusu utulivu wa kifedha inasema hatari ya wastani ilitokana na mazingira mazuri ya uchumi mkuu, ufufuaji wa shughuli za biashara na hatua za kisera zinazochukuliwa na serikali.
Ripoti hiyo pia imesema hatari kwa familia na mashirika yasiyo ya kifedha ilipunguzwa sana, kutokana na kufufuka kwa shughuli za biashara, kuongezeka kwa mapato ya familia, na benki kupunguza masharti ya mikopo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uchumi wa ndani ulikua kwa asilimia 4.7 na asilimia 5.4 mwaka 2022 kwa Tanzania Bara na Zanzibar, mtawalia. Ukuaji huo ulichangiwa kwa kiasi fulani na kufufuka kwa shughuli za kiuchumi, na uwekezaji endelevu wa sekta ya umma na binafsi.