Wizi wa nafaka na mafuta ya Syria, “polisi” amegeuka kuwa “mwizi”?
2023-08-10 14:51:14| CRI

Shirika la Habari la Syria hivi karibuni liliripoti kuwa jeshi la Marekani "limeiba" kiasi kikubwa cha ngano kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuisafirisha kwenye kambi yake ya kijeshi nchini Iraq. Katika miaka ya hivi karibuni, jeshi la Marekani ambalo linajidai kuwa “polisi duniani”, limegeuka kuwa “mwizi wa kimataifa”, na limekuwa likiendelea kupora nafaka na mafuta ya watu wa Syria, na kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya Wasyria.

Ripoti hiyo inasema tarehe 2 mwezi huu, jeshi la Marekani lilisafirisha ngano na mafuta vilivyokusanywa na waasi wa Syria wa eneo hilo na kuvisafirisha hadi katika kambi ya kijeshi ya Marekani kaskazini mwa Iraq kwa kutumia malori 45.

Katika miaka ya hivi karibuni, vyombo vya habari vimeripoti mara kwa mara kwamba jeshi la Marekani linaiba rasilimali kutoka kaskazini mashariki mwa Syria. Tangu mwaka 2014, Marekani imeinglia kati vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, na kupeleka wanajeshi wake kukalia sehemu za mashariki na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Sehemu ya mashariki ndio eneo kuu la uzalishaji wa mafuta nchini Syria. Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aliwahi kutamka hadharani kuwa lengo la kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Syria ni kudhibiti mafuta katika Mashariki ya Kati. Wizara ya Mafuta na Rasilimali za Madini ya Syria ilitoa taarifa kwamba, katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022, wastani wa uzalishaji wa mafuta kwa siku nchini Syria ulikuwa takriban mapipa 80,300, na kati ya hayo, karibu mapipa 66,000 yaliibiwa na “jeshi la Marekani pamoja na waasi wanaoungwa mkono na Marekani katika eneo la mashariki.” Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ilituma barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja huo mwishoni mwa mwaka 2022, ikisema jeshi la Marekani na waasi wa Syria wamesababisha hasara ya moja kwa moja ya dola bilioni 25.9 za kimarekani, ambapo kati ya hizo, dola bilioni 19.8 zilitokana na wizi wa mafuta, gesi asilia na madini. Zaidi ya hayo, hasara isiyo ya moja kwa moja kutokana na kupunguzwa kwa uzalishaji katika sekta ya mafuta, gesi na madini ilizidi dola bilioni 86 za kimarekani. Hasara hizo kubwa zimeongeza maumivu ya watu wa Syria ambayo yamekuwa makubwa sana kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoendelea kwa miaka mingi.

Mkoa wa Hasakah ulioko kaskazini mashariki mwa Syria ni eneo muhimu zaidi la uzalishaji wa nafaka nchini Syria, na zaidi ya asilimia 60 ya nafaka nchini humo zinatoka katika jimbo hilo. Kutokana na jeshi la Marekani, biashara ya chakula kati ya eneo hilo na maeneo yanayodhibitiwa na serikali imezuiwa. Syria ilikuwa nchi inayoweza kuuza chakula nchi za nje, lakini hivi sasa inakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na vita, na inahitaji kuagiza kutoka nje ili kukidhi mahitaji ya ndani.

Kulingana na makadirio ya Shirika la Mipango ya Chakula Duniani, takriban watu milioni 12.4 nchini Syria walikabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula mwaka 2022. Hata hivyo, jeshi la Marekani limeiba bila aibu au hata kuchoma chakula nchini Syria mara nyingi, na kutishia sana haki ya kimsingi ya binadamu ya watu wa Syria.

Jeshi la Marekani linajidai kuwa “polisi wa dunia”. Linaanzisha vita mara kwa mara dhidi ya nchi nyingine kwa visingizio vya “kulinda demokrasia” na “kupambana na ugaidi”, ambapo madhumuni halisi ni kwa ajili ya maslahi yake yenyewe. Popote jeshi la Marekani linapokwenda, halileti amani na ustawi, bali ni vita na majanga yasiyoisha.