Waziri wa Biashara wa China Bw. Wang Wentao na Waziri wa Biashara, Viwanda na Ushindani wa Afrika Kusini Bw. Ebrahim Patel tarehe 10 Agosti waliendesha kwa pamoja mkutano wa nane wa kamati ya pamoja ya biashara kati ya China na Afrika Kusini mjini Pretoria Afrika Kusini, ambako walibadilishana maoni kwa kina juu ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara wa pande nyingi na pande mbili kati ya China na Afrika Kusini, na kufanya maandalizi kwenye sekta ya biashara kwa ajili ya mkutano wa 15 wa viongozi wa nchi za BRICS.
Bw. Wang amesema China inapenda kutekeleza “Pendekezo jipya la uwekezaji” lililotolewa na Afrika Kusini, kupanua uwekezaji kwenye sekta za nishati mpya, uzalishaji viwandani, madini na kilimo, na kudumisha ushirikiano wa mnyororo wa viwanda na ugavi. Amesema China inaitaka Afrika Kusini itoe urahisi na msaada zaidi kwa makampuni ya China ya vifaa vya nyumbani na magari yanayofanya biashara nchini Afrika Kusini.
Bw. Patel amesema Afrika Kusini itaendelea kuboresha mazingira ya kibiashara, kukaribisha makampuni ya China kufanya ushirikiano wa biashara na uwekezaji nchini Afrika Kusini. Amesema Afrika Kusini inataka kupanua zaidi bidhaa za kilimo na viwanda zenye ubora zinazouzwa kwenye soko la China, na kupanua zaidi ushirikiano kwenye mnyororo wa kiviwanda wa magari ya nishati mpya kati ya nchi mbili.