Wizara ya Afya ya Rwanda inapanga kuzidisha nguvu kazi kwenye sekta ya afya mara nne ndani ya miaka minne ijayo, hatua ambayo lengo lake ni kukabiliana na uhaba wa wauguzi na wakunga nchini humo.
Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa wizara ya Afya ya Rwanda Theophile Dushime, amesema kwa sasa mtaalamu mmoja tu mwenye ujuzi ambaye kwa sasa anahudumia watu 1,000, lakini mahitaji ni walau wataalamu watano kwa kila watu 1,000. Amesema kwa sasa kuna robo tu ya wauguzi wanaohitajika nchini Rwanda.
Ameongeza kuwa lengo hilo litafikiwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaohitimu masomo ya udaktari, uuguzi, na wakunga kutoka 2,000 hadi 8,000 kila mwaka.
Kwa sasa kuna vituo vya afya 1,247, zahanati 512, hospitali za wilaya 40, hospitali nne za mkoa, na hospitali nane za rufaa nchini kote Rwanda.