Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuchukua hatua kukabiliana na maafa ya mara kwa mara Ziwa Victoria
2023-08-13 22:04:30| cri

Jumuiya ya Afrika Mashariki imetakiwa kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti majanga yanayozidi kutia wasiwasi katika Ziwa Victoria. Hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa haraka ni pamoja na ujenzi wa vituo vya uokoaji kwenye visiwa katika eneo la maji linalomilikiwa kwa pamoja na Tanzania, Uganda na Kenya.

Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia tume ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), imesema hatua hiyo ni muhimu na inaweza kusaidia kuokoa maisha ya watu. Wiki mbili tu zilizopita waumini 14 wengi wao wakiwa ni watoto walikufa maji wilayani Bunda, mkoani Mara, Tanzania baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka kutokana na upepo mkali. Siku moja baadaye wavuvi wengine 20 walikufa maji upande wa Uganda.

Ajali zote mbili zilitokana na upakiaji kupita kiasi na hali mbaya ya hewa. Ziwa Victoria ambalo ni ziwa kubwa zaidi barani Afrika, limeshuhudia maafa mengi ya aina hiyo yanayosababisha vifo vya mamia ya watu. Inakadiriwa kuwa karibu watu 5,000 hupoteza maisha kila mwaka katika ziwa hilo.